Jumatatu , 15th Dec , 2014

Jeshi la Polisi mkoani Kagera limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Jeshi la Polisi mkoani Kagera limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wakiandamana huku wakifurahia ushindi walioupata katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza mara baada ya kuwatawanya wananchi hao Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera Henry Mwaibambe amesema jeshi hilo lilipiga marufuku wananchi kuandamana bila kibali maalumu na kusabisha vurugu zisizo kuwa za lazima mitaani na akaongeza kuwa chama chochote kitakachofanya maandamano bila kibali maalumu kitachukuliwa hatua za kisheria.

Nao baadhi ya wananchi ambao walikuwa katika maandamano hayo wamesema maandamano yao yalikuwa ya amani na walikuwa wanafurahia ushindi walioupata katika uchaguzi huo na kwamba sasa wameamua kufanya mabadiliko kwa kuwa wamechoshwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwakuwa imekuwa ikiwafumbia macho viongozi wa chama hicho ambao wameshiriki katika wizi wa pesa za Escrow huku wananchi wakiendelea kubaki masikini.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA katika manispaa ya Bukoba Victor Sherejey amesema sasa wakati umefika wakufanya mabadiliko na wameibuka na ushindi katika mitaa 30 kati ya mitaa 66 iliyoko katika manispaa hiyo.