Jumamosi , 24th Sep , 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi wanaozunguka eneo la uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi wanaozunguka eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro kati yao na mwendeshaji wa uwanja huo kampuni ya KADCO.

Prof Mbarawa mgogoro huo uliopo kati yao na mwendeshaji wa uwanja huo kampuni ya KADCO, ufumbuzi utakaopatikana utakuwa na manufaa kwa pande zote na kujali maslahi ya Taifa.

"Msiwe na wasiwasi Serikali yenu ni sikivu, tutayakagua maeneo yote na kuangalia maslahi ya pande zote na kutoa maamuzi yenye manufaa kwa wote", amesisitiza Prof. Mbarawa.

Mgogoro kati ya wananchi wanaozunguka uwanja wa ndege wa KIA na kampuni ya KADCO ambao umekuwako toka mwaka 1998 umesababisha misuguano na hisia kali kwa muda mrefu hali iliyosababisha Serikali kuamua kuupatia ufumbuzi wa kudumu.

Waziri Prof. Mbarawa ametuma timu ya wataalamu kupitia eneo lote la uwanja wa ndege huo lenye kilomita za mraba 110 katika siku mbili kuanzia sasa ili kuangalia wadau wote walioko ndani ya eneo hilo, athari zake kwa uwanja na wananchi kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa ameitaka KADCO kuongeza mapato katika uwanja wa ndege wa KIA ambao ni wa pili kwa ukubwa hapa nchini ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza mapato katika sekta zote za kiuchumi.