Alhamisi , 26th Mei , 2016

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ameivunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Waziri prof Ndalichako amefanya uteuzi kwa watu wawili kushikilia TCU kwa muda wakati uchunguzi ukiendelea ambao ni Profesa Eleuther Mwageni kukaimu nafasi ya Katibu Mtendaji akitokea katika nafasi ya Naibu Makamu Mkuu Utawala na Fedha wa Chuo Kikuu cha Ardhi.

Mwingine ni Dk. Kokubelwa Moleli ambaye anapewa nafasi ya Ukurugenzi wa Udahili na Nyaraka na kabla ya uteuzi huo alikuwa Mratibu wa Idara ya Elimu ya Juu.

Wakati waliosimamishwa kupisha uchunguzi ni Katibu Mtendaji Profesa Yunus Mgaya, kushindwa kutekeleza wajibu wake kama mtendaji mkuu wa taasisi, Dk. Savinus Maronga Mkurugenzi wa kutoa ithibati kwa vyuo vikuu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusmamia ubora na ithibati ya vyuo vikuu.

Wengine ni Mkurugenzi wa udahili, Rose Kishweko kwa udahili wa wanafunzi wasio na sifa na Kimboka Istambuli ambaye alikuwa kaimu mkurugenzi wa udahili.

Mwenyekiti wa TCU Awadhi Mawenya, alisimamisha kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kuwadahili wanafunzi hao.

Hata hivyo Profesa Ndalichako, ametuma salamu kwa wanafunzi hewa ambao wako vyuoni huku wakiendelea kutafuna fedha za mikopo kuwa dawa yao ipo jikoni na imeshachemka na wakati wowote atakabiliana nao kwa kushirikiana na Takukuru.

Sauti ya Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,Profesa Eleuther Mwageni,