Jumanne , 26th Mei , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua makatibu tawala wa Mikoa ya Singida na Shinyanga kuanzia jana, Jumatatu, Mei 25, 2015.

Katika uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua Ndugu Festo Luganda Kang’ombe kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida na Ndugu Abdul Rashid Dachi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga.

Kabla ya uteuzi wake, Ndugu Kang’ombe alikuwa Mkurugenzi wa Halmashuri ya Kibaha, Mkoa wa Pwani wakati Ndugu Dachi alikuwa Katibu Tawala Msaidizi, Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi.

Ndugu Kang’ombe anachukua nafasi ya Ndugu Liana Hassan ambaye amestaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria tokea Machi, mwaka huu, na Ndugu Dachi anachukua nafasi ya Ndugu Anselm Tarimo ambaye naye alistaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria Januari 22, mwaka huu, 2015.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
26 Mei, 2015