Jumatatu , 30th Mar , 2015

Vijana wa Afrika wamemtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete moja ya tuzo kubwa zaidi zinayotolewa na vijana wa Afrika kwa kutambua uongozi wake bora na mchango wake katika kuendeleza vijana.

Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Tuzo hiyo iitwayo The African Youth Peace Award hutolewa na Umoja wa Vijana wa Afrika wa Pan Africa Youth Union kwa wakuu wa nchi na viongozi wa Afrika ambao wamethibitika kuchangia sana kwa ustawi wa Waafrika.

Rais Kikwete alikabidhiwa tuzo hiyo na Rais wa Pan African Youth Union, Bi. Francine Furaha Muyumba wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wakati Rais aliposimama kwa dakika chache kuwasalimia vijana wanaohudhuria Mkutano wa Tatu wa Viongozi Vijana wa Afrika na China (3rd Africa-China Young Leaders Forum) ulioanza jana, Jumamosi,katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Ngurdoto, Arusha.

Katika salamu zake za utangulizi, Bi. Muyumba alimweleza Rais Kikwete kama kiongozi mfano wa kuigwa kwa mchango wake katika kuwatambua na kuwaendeleza vijana katika nafasi za uongozi.

Kabla ya kuwasalimia vijana hao, Rais Kikwete ambaye alitembelea Arusha kwa saa chache kabla ya kurejea Dar es Salaam, alikutana kwa mazungumzo na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Zimbabwe, Mheshimiwa Robert Gabriel Mugabe, ambaye alikuwa Arusha kufungua Mkutano huo wa Africa-China Young Leaders Forum jioni ya jana hiyo.

Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete alimshukuru Rais Mugabe ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuia ya Mandeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kukubali mwaliko wake wa kutembelea Tanzania, ili kufungua Mkutano huo wa siku mbili. Mkutano huo unaandaliwa kwa pamoja na Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wa Chama cha Kikomunisti cha China.

Mkutano huo wa Africa-China Young Leaders Forum ni wa tatu lakini unafanyika nchini kwa mara ya kwanza. Mikutano miwili ya kwanza ilifanyika Windhoek, Namibia na Beijing, China.

Mbali na Tanzania na China, nchi nyingine za Afrika zinazohudhuria Mkutano huo ni Angola, Kenya, Uganda, Sudan, Shelisheli, Afrika Kusini, DRC, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Eritrea, Burundi, Namibia na Niger.

Rais Kikwete pia alikutana kwa mazungumzo na Mheshimiwa Wang Jiariu, Makamu Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa vijana kutoka China kwa ajili ya Mkutano huo.

Rais Kikwete amemshukuru Mheshimiwa Jiariu kwa heshima ambayo vijana wa Afrika na China wameipa Tanzania na Chama cha Mapinduzi kwa uamuzi wao wa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huo.