Jumamosi , 25th Sep , 2021

Mkuu wa mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge, amesema kuwa umebaki mwezi mmoja tu kufikia tarehe ya mwisho ya matumizi ya chanjo ya COVID-19 iliyotolewa ndani ya mkoa huo na kwamba wameanzisha mpango shirikishi utakaowasaidia wananchi kupata chanjo kwa hiari yao popote walipo.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge

Kauli hiyo ameitoa hii leo Septemba 25, 2021, na kusema kuwa mkoa huo ulipokea jumla ya dozi za chanjo 30,000 lakini hadi sasa ni dozi 15,000 tu ndiyo zilizotumika na hivyo ipo haja ya kutumia mbinu shirikishi ili wananchi wachanjwe kabla ya tarehe ya mwisho ya matumizi ya chanjo haijafika.

"Chanjo 15,000 zilizobaki zimebakisha mwezi mmoja ziharibike na hazitatumika tena baada ya muda huo, hivyo wananchi wenye utayari wajitokeze na kuokoa chanjo iliyobaki kuokoa maisha yao na chanjo isiharibike" amesema RC Kunenge.