Jumanne , 9th Feb , 2016

SACCOS moja mjini Makambako mkoani Njombe yadaiwa kushindwa kutoa pesa kwa wanachama wake hali iliyozua taharuki na kuzusha madai ya taasisi hiyo kuwa huenda imefilisika.

BAADHI ya wakazi na vikundi vya wajasiriamali mji mdogo wa Makambako wamelalamikia kutopata pesa zao walizo ziweka kama akiba katika Saccos ya Makambako na kuomba mrajisi wa ushirika kuchunguza kama pesa zao zipo na kama hazipo kutaifisha mali za Saccos ili kurejeshewa pesa zao.

Wakizungumza kwa masikitiko baadhi ya wananchi waliojiwekea pesa zao katika Saccos hiyo kwa nyakati tofauti mjini Makambako wamesema kuwa wameshindwa kulipa ada za watoto wao kutokana na Saccos hiyo kutokuwa na fedha na kila wanapokwenda kuambiwa wasubiri ama kuambiwa warudi siku nyingine na mara nyingine kupewa pesa kidogo kidogo.

Wamesema kuwa wanamuomba mrajisi wa vyama vya ushirika kufika katika Saccos hiyo ili kuzinusuru pesa zao na kuwa waliamini kujiwekea akiba katika Saccos hiyo lakini inavyowafanyia wanahisi imefirisika.

Baadhi ya wanachama walioeleza masikitiko yao ni Fatuma Sharima mamalishe, Claud Mwinuka Mwanakikundi, Aldofu Msiliga, Mwanachama, Prisca Amri.

Baada ya kufika katika ofisi ya Saccos hiyo meneja wake amedai kuwa yeye sio msemaji na kusema kuwa mwenyekiti wa bodi ndiyo msemaji wa Saccos hiyo lakini hakuwepo na alikuwa nje ya ofisi huku akikili kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kuwapa walio weka akiba.

Naye afisa ushirika wa halmashauri ya mji Makambako aliondoka ofisini kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari na baada ya kupigiwa simu yake haikupatikana licha ya mweyekiti wa halmashauri kukiri kuwepo kwa suala hilo.