Jumamosi , 18th Sep , 2021

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka, ameitaka Wizara ya Afya kuacha sinema za maonesho kwa kutoa ahadi zisizo na matokeo yanayoonekana kwa wananchi kwa kushindwa kumlipa hati za malipo takribani 4 mkandarasi anayejenga hospitali ya kanda Mtwara.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka

Shaka amesema kuwa pamoja na kasi nzuri ya ujenzi inayofanywa na mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa, lakini Wizara ya Afya, imekuwa kikwazo kikubwa katika kuhakikisha hospital hiyo inakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

"Naitaka Wizara ya Afya kueleza kama walimdanganya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango alipofika kuweka jiwe la msingi kwamba mapema mwezi Oktoba hospitali hii itakuwa imeanza kutoa huduma lakini ajabu mpaka leo hakuna dalili hizo, sasa ni vizuri wabadilike waanze kuwa watendaji badala ya kuwa wapiga maneno matupu," amesema Shaka.