Alhamisi , 23rd Jun , 2022

Vijana wa Kitanzania zaidi ya 5,000 wenye vipaji na wabunifu wanatarajiwa kupata ufadhili wa masomo kutoka kwenye Taasisi ya Ruge Mutahaba, itakayozinduliwa rasmi usiku wa Jumapili ya Juni 26, 2022.

Mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Taasisi ya Ruge Mutahaba Georgia Mutagahywa

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa bodi ya wadhamini wa taasisi hiyo Georgia Mutagahywa, na kubainisha kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuwaunganisha vijana mbalimbali wa Tanzania na kuwawezesha kuchangamkia fursa zilizopo katika jamii zao.

Akizungumza kwa niaba ya vyombo vya habari vitakavyoshiriki katika uzinduzi wa taasisi hiyo Reuben Ndege, amesema vyombo vya habari vimejitolea kushirikiana na taasisi hiyo kama moja ya njia ya kuenzi mchango wa Ruge katika tasnia ya habari na burudani.

Rwebu Mutahaba akiiwakilisha familia ya marehemu Ruge Mutahaba ameshukuru kwa ushirikiano mkubwa ambao wameendelea kuupata kutoka kwa wadau mbalimbali hasa katika kuyaendeleza maono aliyokuwa nayo Ruge.

Rwebu Mutahaba, mwakilishi wa familia ya marehemu Ruge Mutahaba

Ni miaka mitatu tangu Ruge Mutahaba alipofariki na taasisi hiyo katika kumuenzi itajikita katika ubunifu, uvumbuzi, umahili, upambanaji na uzalendo kwa vijana na matangazo ya uzinduzi wa taasisi hiyo yatarushwa katika vyombo mbalimbali ikiwa ni pamoja na East Africa TV.