Jumanne , 23rd Aug , 2016

Wanasayansi nchini wametakiwa kufanya tafiti zitakazoiwezesha serikali kuongeza uzalishaji na kutatua changamoto za utoaji huduma katika jamii na kuchochea maendeleo.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako akitembelea maonesho ya wanasayansi mara baada ya kufungua Kongamano la Tano la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifujijini Dar es Salaam leo.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako ameitaka tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuhakikisha tafiti wanazofanywa zijikite katika kutoa matokeo yatakayoweza kutatua matatizo ya wananchi, kutengeneza ajira ili kuinua kipato cha wananchi na uchumi kwa ujumla.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kuzindua Kongamano la Tano la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambapo amesema kuwa kufanya hivyo kutasaidia katika Kutekeleza agizo la Uchumi wa viwanda kwa kupata rasilimali watu wenye ufahamu na ubunifu katika uzalishaji wenye tija.

Profesa Ndalichako amesema kuwa kumekuwepo na tafiti za Kilimo zilizofanywa na taasisi mbalimbali ambazo zimefanikiwa kutoa matokeo mazuri zikiwemo za utengenezaji wa mbegu bora zinazoongeza mavuno kama vile mbegu za mihogo, mahindi na mpunga ambazo zinavumilia ukame na zinaweza kukinzana na magonjwa.

“Tumeona matokeo chanya katika uvumbuzi wa 'software' zilizobuniwa na vijana wetu hapa nchini ambazo tunatumia na zinarahisisha utendaji na kuokoa muda, siyo hilo tuu pia vijana wetu wameweza kutengeneza injini ya treni ambazo nazo zitasaidia katika shirika letu la reli, yapo mengi sana tuna ya thamini na tutayaendeleza,” amesema Prof. Ndalichako

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)Dkt. Hassan Mshinda amesema kuwa tafiti ambazo zinagharamiwa na tume hiyo tayari zimeanza kuwasaidia wananchi katika maeneo mbalimbali ukiwemo Mkoa wa LINDI.

“Kwa kupitia tafiti zetu tumeweza kupata chanjo inayozuia magonjwa ya kuku kama vile mdondo, ndui na mafua katika chuo Kikuu cha Sokoine, chanjo ambazo zitawasaidia wafugaji wa kuku” alisema Mshinda.

Kongamano la Tano la Kitaifa la Sayansi Teknojia na Ubunifu litafanyika Jijini DSM kwa Siku TATU na litatoa fursa kwa wataalamu wakiwemo watafiti, wabunifu, watunga sera na wajasiriamali kukutana na kujadili mchango wa sayansi.