Jumatano , 16th Jul , 2014

Serikali ya Tanzania imesema inachukua tahadhari ya kuzuia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kwa wananchi wake hasa wanaoishi katika maeneo ya mipakani kwa lengo la kujizuia kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

Mganga mkuu wa serikali Dkt Donan Mmbando (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt Servacius Likwelile.

Mganga mkuu wa serikali Dk. Donald Mbando amesema tahadhari hiyo inafuatia kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi za afrika magharibi na hivyo serikali imeshatuma timu ya wataalam wake katika maeneo ya mipakani kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi ya namna ya kumgundua mtu mwenye virusi vya ugonjwa huo.

Dk. Mbando amesema kupitia wataalam wa afya waliopo katika mipaka ya nchi serikali itakuwa ikitoa taarifa za mara kwa mara ya namna uzuiaji wa ugonjwa huo kwa wananchi na wanapata elimu ya kutosha ya kujikinga na virusi vya Ebola.

Wakati huo huo, uchunguzi wa East Africa Radio umebaini kuwepo kwa matumizi makubwa ya mashine zinazodaiwa kupima na kutambua magonjwa mbali mbali ya binadamu za Guantamo Analyzer, mashine ambazo sifa na uwezo wake katika kubaini magonjwa inayopima ni wa kutiliwa shaka.

Mashine hizo zimekuwa zikitumiwa kwa wingi na watu wanaodai kutoa tiba mbadala ambapo mbali ya kupima na kutambua orodha kubwa ya homa na magonjwa yanayowasumbua wanadamu, mashine hizo pia zinadaiwa kuwa na uwezo wa kuondoa sumu mwilini.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu mashine hizo, msajili wa bodi ya maabara binafsi Bi. Zainab Mfaume amekana kuzifahamu na kwamba hazipo katika orodha ya vifaa vya uchunguzi wa magonjwa vinavyotambuliwa na bodi hiyo.