Jumatano , 16th Jul , 2014

Chama cha wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo Tanzania kimesema jitihaha za serikali katika kusaidia ajira kwa vijana haziwezi kufikiwa endapo mipango itaandaliwa kisiasa bila kuwa na malengo yanayopimika na kushirikisha sekta binafsi.

Waziri wa viwanda na Biashara nchini Tanzania Dkt Abdallah Kigoda.

Akiongea katika ufunguzi wa baraza la wafanyabiashara jijini Mbeya Makamu Rais wa chama hicho Julius Kaijage amesema kuwa mpaka sasa hakuna mipango thabiti inayolenga kutatua changamoto za vijana katika sekta mbalimbali na kwamba vijana wengi wanapoteza mwelekeo kutokana na kutoandaliwa vyema hasa katika kuwajengea uwezo na ujuzi wa kujiajiri na kujitegemea.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abass Kandoro amesema uwekejzaji wa ndani ukipewa nafasi unaweza kuleta mabadiliko chanya na kuzalisha ajira nyingi kwa watanzania kupitia fursa na rasilimali zilizopo ambazo zinahitaji kujengewa mazingira mazuri kati ya taasisi na umma na binafsi.

Kandoro ameongeza kuwa serikali haifanyi biashara ila inatoa nafasi na kuziwezesha sekta binafsi katika kuharakisha ukuaji wa uchumi wa nchi na kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana hapa nchini.

Wakati huo huo serikali imekiri kuwepo kwa uzembe katika kuchangamkia soko la nyama ya mbuzi katika nchi za kifalme za kiarabu ambako kuna uhitaji mkubwa wa nyama hiyo.

Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk, Rehema Nchimbi, wakati akifungua kongamano la miradi ya maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2014 mjini Dodoma.

Dk, Nchimbi amesema kumekuwepo kwa uzembe mkubwa kutoka kwa watendaji ambao wameshindwa kutumia fursa hiyo ya kuuza nyama ya mbuzi kwenye nchi za falme za kiarabu hata mara baada ya nchi hizo kuonyesha uhitaji mkubwa wa nyama ya mbuzi kutoka nchini.