Jumatatu , 15th Feb , 2016

Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) imekifungia kwa muda usiojulikana kiwanda cha kukamua mafuta yanayotokana na mbegu za pamba cha Yobama Shirecu kilichopo kata ya Lugulu wilayani Itilima kutokana na kutumia malighafi zenye sumu.

Mkaguzi mwandamizi TFDA kanda ya Ziwa Julius Panga

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa zaidi ya magunia 600 ya mbegu zisizofaa yamegundulika , huku lita 520 za mafuta zikifikishwa polisi kama ushahidi.

Akiongea na Eatv baada ya kukagua uzalishaji wa mafuta na kufikia uamuzi wa kukifungia kiwanda hicho Mkaguzi mwandamizi TFDA kanda ya Ziwa Julius Panga amesema kuwa wamefunga kiwanda hicho kutokana na kutumia mbegu zenye sumu ambazo ziliandaliwa kwa ajili ya msimu wa kilimo na siyo kukamua mafuta.

Panga amesema kuwa malighafi inayotumia kutayarishia mafuta katika kiwanda hicho haikidhi ubora na usalama, ambapo mbegu zina dawa kwa ajili ya kupandwa shambani pia mazingira ya kiwanda hicho si rafiki kwa mlaji wa bidhaa hiyo.

Aidha mkaguzi huyo ametoa wito kwa wanunuzi na walaji kuhakikisha wanaangalia muda wa kuisha matumizi ya bidhaa na pindi wanapobaini ni vema wakatoa taarifa kwa mamlaka husika.

Kwa upande wake afisa usafi na mazingira wilaya ya Itilima Kelisa Wambura amesema ameunga mkono hatua zilizochukuliwa na TFDA na kuahidi kusimamia agizo hilo.

Naye afisa afya wa mkoa wa Simiyu, Makoye Madaraka amewataka wananchi kutoa ushirikiano ili kubaini viwanda bubu ili kuhakikisha wote wanaotengeneza chakula kwa malighafi ambayo ni hatarishi wanachukuliwa hatua sitahiki .

Jumla ya dumu 52 za lita kumi kumi za kuhifadhiwa mafuta zilikamatwa na kupelekwa polisi kwa uchunguzi zaidi.