Jumatano , 25th Mei , 2016

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema inatiwa wasiwasi na ongezeko la ghasia kufuatia maandamano ya kila wiki nchini Kenya.

Waandamanaji wakijaribu kukimbia Polisi waliokuwa wanarusha mabomu ya Machozi

Kwa mujibu wa ofisi hiyo jana watu watatu wameripotiwa kuuawa , wawili wakipigwa risasi na polisi mjini Siaya Magharibbi mwa Kenya karibu na mpaka na Uganda huku mmoja akidaiwa kuuawa na polisi mjini Kisumu.

Watu wengine wengi wakiwemo polisi wamearifiwa kujeruhiwa huku, Maandamano yaliripotiwa kuzuka pia katika miji mingine ikiwemo mji mkuu Nairobi.

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Rupert Colville amesema umoja huo unaitaka serikali ya Kenya kuhakikisha vitendo hivi vya ghasia havijirudii na kuheshimu haki ya kukusanyika kwa amani.

Pia ametoa wito kwa waandamanaji kuandamana kwa amani na kutojihusisha na ghasia kama ambavyo imejitokeza wiki iliyopita na katika maandamano ya wiki hii.

Ofisi ya haki za binadamu imeongeza kuwa picha na video zikionyesha polisi wanavyo wapiga na kuwaadhibu waandamanaji inazua maswali endapo vikoso vya usalama Kenya vinazingatia sheria za kimataifa dhidi ya matumizi ya nguvu kupita kiasi.