Jumatano , 27th Apr , 2016

Mhadhiri wa Chuo cha Sayansi ya Tiba cha Muhimbili Dkt. Ave Maria Semakafu amesema kwamba suala la usawa wa kijinsia katika kupewa nafasi za kuongoza sekta mbalimbali ni vyema likawekwa kwenye katiba ili kila Rais atakayechaguliwa aweze kuifuata.

Dkt. Semakafu ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Wanawake Live kinachorushwa na kituo cha EATV.

Suala na mgawanyo wa nafasi za uongozi kati ya wanawake na wanaume bado halipo kikatiba ndiyo maana ukiangalia nafasi nyingi alizofanya uteuzi Rais Magufuli wanawake ni wachache sana ukilinganisha na huko tulikotoka katika serikali ya awamu ya nne.

''Usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi ukiwa katika katiba utamfanya kila kiongozi wa nchi atakayechaguliwa kuhakikisha anazingatia mfumo huo kuliko ilivyo sasa''-Amesisitiza Semakafu

Mwanaharakati huyo wa kutetea haki za wanawake nchini ameongeza kuwa katika uongozi inatakiwa mtu apewe nafasi kulingana na uzoefu wake na si iwe kama upendeleo au kwa kigezo cha kuzingatia jinsia.

''Kuna wanaume wengi wana vyeo mfano Profesa, au Daktari utasikia mwanaume anatajwa kwa cheo chake ila ikifikia upande wa mwanamke anatajwa kwa jina Mama Semakafu hii huondoa dhana ya kuleta usawa katika cheo hicho''- Ameongeza Semakafu.