Alhamisi , 16th Nov , 2017

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Asha Abdallah, amesikitishwa na hali ya vifo vya watoto njiti ambavyo hutokea zaidi siku chache baada ya kuzaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya watoto njiti yanayoadhimishwa Novemba 17 kila mwaka, amesema katika Hospitali ya Mnazi mmoja pekee, watoto 347 waliofariki, 154 walikuwa ni njiti.

Alisema idadi ya watoto njiti wanaozaliwa inaongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mimba za utotoni.

Amesema idadi ya watoto njiti waliolazwa hospitali kwa huduma maalumu ya kangaroo, imeongezeka kutoka 215 mwaka 2015 hadi 771 mwaka 2017.

Ameeleza sababu za kuzaliwa watoto njiti ni matatizo yanayoambatana na ujauzito yakiwamo shinikizo la damu, kisukari, matatizo ya mfuko wa uzazi na unene uliokithiri.