Ijumaa , 18th Jul , 2014

Mwanaharakati maarufu barani Afrika ambaye ni raia wa Kenya Profesa PLO Lumumba, amesema tatizo la rushwa katika nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Tanzania linatokana na viongozi wa nchi hizo kukosa utashi wa dhati wa kisiasa.

Mwanaharakati maarufu barani Afrika ambaye ni raia wa Kenya Profesa PLO Lumumba.

Akizungumza na East Africa Radio, Profesa Lumumba amesema inashangaza kuona wala rushwa wakubwa hawashughulikiwi na vyombo vya sheria, kiasi baadhi yao wanajipenyeza katika siasa na hata kuwa viongozi wa nyadhifa za juu katika serekali za nchi husika.

Profesa Lumumba ambaye amewahi kushika wadhifa wa Mkuu wa Tume ya Kupambana na Rushwa nchini Kenya, amesema kuna haja ya nchi za Afrika kuongeza ukomavu wa kidemokrasia kwa kuacha kuingiza siasa katika mapambano ya rushwa na badala yake waache sheria ichukue mkondo wake.

Hapo jana, Profesa Lumumba aliwasihi wajumbe wa bunge maalumu la katiba kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA kurejea bungeni na kuendelea na mchakato wa katiba mpya.

Profesa Lumumba ambaye pia ni mkuu wa bodi ya wakurugenzi wa shule kuu ya Sheria nchini Kenya, alikuwa akizungumza kama mjumbe wa jopo maalumu lililoundwa na Jukwaa la Katiba kwa ajili ya kusuluhisha na kunusuru mchakato wa katiba mpya.

Katika maelezo yake Profesa Lumumba amesema idadi kubwa ya watu, wanasiasa na wadau wa katiba waliohojiwa na jopo hilo wamependekeza UKAWA warejee bungeni sambamba na kulitaka bunge hilo lijadili na kuheshimu rasimu ya katiba iliyo mbele yao pamoja na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kuacha lugha ya matuzi, kebehi na fedheha.