Jumamosi , 18th Apr , 2015

Zaidi ya wafanyabiashara 700 wa madini, kutoka nchi mbalimbali duniani, wanatarajiwa kushiriki maonesho ya Kimataifa ya madini ya vito na usonara ya Arusha (AGF), mapema wiki ijayo, Jijini humo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Maonyesho, Peter Pereira

Katika maonesho hayo zaidi ya waonyeshaji 60 kutoka bara la Afrika, watashiriki kwa kuonesha na kuuza madini hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Maonyesho hayo, Peter Pereira amesema jana jijini humo, kuwa maonesho hayo yatakuwa ya siku tatu, ambapo yataanza April 21 hadi 23, mwaka huu.

Amesema wanatarajia wafanyabiashara wa madini ya vito, watapata fursa ya kukutana na wauzaji madini wa nje ya nchi na kukutana na wanunuzi wakubwa, hatua itakayojenga mahusiano ya kibiashara baina yao.

Amezitaja nchi wanazotoka wafanyabiashara hao kuwa ni pamoja na China, Thailand, Marekani, India, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Canada, Japan na Urusi.

Pia amezitaja nchi wanazotoka waoneshaji wa bara la Afrika ni Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Msumbiji, Rwanda, DRC na Kenya.

Pereira amesema baadhi ya aina ya madini yatakayokuwepo kwenye maonesho hayo, yanayoandaliwa na serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini, kwa kushirikiana na Chama cha Wauza Madini Nchini (TAMIDA) na Tanzanite kuwa ni Rodlife, Opal (Kigoma), Rubi (Longido), Amaroy (Babati), Redlight, Green Tomaline, Almasi na mengineyo yenye ubora na thamani kubwa.

Mwenyekiti huyo amesema pamoja na kushiriki kwenye maonesho hayo, washiriki watapata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii, kama vile Hifadhi ya Ngorongoro na Mbuga za wanyama na pia kutembelea machimbo ya Tanzanite Mererani.