Jumatano , 24th Sep , 2014

Wafuasi watano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Ernest Mangu.

Wafuasi hao akiwemo Mratibu wa Chadema Kanda ya Magharibi, Christopher Nyawanji wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Verynice Kawiche.

Washtakiwa wengine ni Laurent Manguweshi ambaye ni katibu wa Chadema Mkoa wa Katavi, Agnes Stephano mkazi wa Dar es Salaam, Elisha Daudi Mkazi wa Tabora na Tuli Kiwanga ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Mkoa wa Dodoma.

Akisoma mashitaka hayo, wakili wa Serikali, Chivanenda Luongo alidai watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 18 mwaka huu katika Manispaa ya Dodoma.

“Watuhumiwa wanashitakiwa kwa mashitaka mawili la kufanya mkusanyiko usiokuwa halali na kukaidi amri halali ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya kutowataka waandamane,” alisema.

Washitakiwa hao ambao wanatetewa na mwanasheria Tundu Lissu wamekana mashitaka yao na wako nje kwa dhamana hadi kesi yao itakapotajwa tena Oktoba 22 mwaka huu.

Akizungumza nje ya mahakama, Lissu amesema watuhumiwa hao walikuwa wanatoka Dar es Salaam kwenye mkutano mkuu wa chama wakielekea kwao.