Jumanne , 24th Mar , 2015

Wakati msako wa kuwakamata waganga wapiga ramli chonganishi ukiendelea nchi nzima hasa katika mikoa ya kanda ziwa, jeshi la polisi nchini limepewa onyo toka kwa wanganga wa jadi juu ya vifaa vinavyokamatwa wakati wa msako wao.

Jeshi hilo limepewa tahadhali ya kukumbana na hatari yeyote baadaye ikiwa wataendelea kukamata vifaa hivyo vikiwamo vibuyu, vitambaa vyeupe na vyeusi, ngao, mikuki pamoja na shanga huku likitakiwa kurejesha mara moja baadhi ya vifaa hivyo ambavyo vimekamatwa.

Katibu mwenezi wa chama cha waganga wa tiba asili nchini, (Chawatiata), Steven Sebastian kutoka Mwanza, akizungumza katika mkutano wa waganga wa jadi wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu, amesema kitendo cha kuchukua vibuyu vyao, kutawafedhehesha.

Sebastiani akizungumza mbele ya kamanda wa polisi mkoani hapa, Charles Mkumbo, amesema kitendo kinachofanywa na jeshi hilo cha kukamata vifaa hivyo, ni kitendo cha hatari kwani kinaweza kusababisha hali ya migogoro mikubwa kati ya jeshi la polisi na jamii.

Sebastian alieleza vibuyu, vitambaa vyeupe, na vyekundu, shanga, ngao, pamoja na mikuki ni vifaa ambavyo waganga hao walirithishwa na wazee wa zamani ambao alieleza vifaa hivyo walivitumia katika kutafuta uhuru.

Akizungumzia hilo, kamanda wa polisi Mkumbo amesema siyo kweli waganga wa jadi wanaonewa ama kusingiziwa wanapiga ramli chonganishi, bali kutokana na uchunguzi wao wamebainika kuwapo na hali hiyo.