Jumatatu , 8th Aug , 2016

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha amesema sekta ya kilimo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka minne mfululizo nchi imeweza kuzalisha chakula cha ziada, ambapo kwa mwaka huu imezalisha kwa asilimia 123.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha

Ole Nasha ametoa taarifa hiyo leo katika sherehe za maadhimisho ya Sikukuu ya Nanenane ambazo zimefanyika Jijini Mbeya, kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini.

“Mafanikio hayo yanachangiwa jitihada za Serikali katika kutoa ruzuku ya pembejeo, taasisi za utafiti ambazo zimekuwa zikitafiti aina bora ya mbegu zikitafuta mbegu bora na wakulima walioamua kuwekeza kwenye kilimo,” amesema.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema katika ukanda wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni nchi mbili tu za Tanzania na Zambia kati ya nchi 15 za jumuiya hiyo hazikabiliwiu na baa la njaa.

Licha ya mafanikio hayo Naibu Waziri huyo aliwaomba wakulima kuendelea kuzalisha kwa kufuata kanuni bora za kilimo pamoja na kutumia pembejeo bora.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ladislaus Mwanakatwe ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuwatetea pamoja na utatuzi wa kero za muda mrefu zilizokuwa zinawakabili wakulima ikiwemo ya tozo.

Hata hivyo Mwanakatwe ameiomba serikali kuitafutia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo.

Pia ameomba serikali iwezeshe Benki ya Kilimo (TADB) kufungua matawi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili wakulima wake waweze kupata mikopo kwa urahisi.