Alhamisi , 25th Jun , 2015

Wagombea wa Urais kupitia CCM wameendelea kurudisha fomu zao baada ya kukamilisha zoezi la kutafuta wadhamini katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Jengo la Makao makuu ya Chama Tawala nchini Tanzania Chama cha Mapinduzi (CCM).

Waliorejesha fomu mapema siku ya leo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mathias Chikawe, Waziri wa Maendeleo mifugo na uvuvi, Dk, Titus Kamani na Boniface Ndengo.

Wagombea hao walitumia muda wao wakati wanaongea na waandishi wa habari kuwashukuru wanachama wote waliojitokeza kuwadhamini huku wakikiri uwepo wa rushwa katika zoezi zima la kutafuta wadhamini hao mikoani.

Hata hivyo Waziri Chikawe alikataa kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu zake kwa madai kuwa hakujipanga kuzungumza nao.

Mpaka sasa ni wagombea urais nane tu ambao wamerejesha fomu zao baada ya kukamilisha zoezi la kuwatafuta wadhamini mikoani.