Alhamisi , 16th Jul , 2015

Wanachama mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma wamejitokeza leo kuchukua fomu za kuwania ubunge na udiwani kupitia chama hicho.

Jengo jipya la Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Dodoma.

Katika ofisi za CCM Wilaya za Dodoma Mjini na Chamwino kulikuwa na idadi kubwa ya wanachama waliofika kuchukua fomu huku wakiahidi kutelekeza ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Mpaka mchana wa jana ni wanachama wawili tu wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge kwenye jimbo la Dodoma mjini ambao ni mbunge aliyemaliza muda wake, David Malole na mfanyabiashara anayemiliki kiwanda cha magodoro ya Dodoma asili mjini hapa, Haidari Gulamali.

Katika Jimbo la Chilolwa ambalo liko Wilayani Chamwino na ambalo mbunge aliyemaliza muda wake, Hezekia Chibulunje ameshatangaza kutowania nafasi hiyo kwa mwaka huu wamejitokeza wanachama sita kuwania jimbo hilo mpaka mchana wa leo.

Waliojitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Joel Makanyaga, Daniel Ligoha, Anderson Magolola, Deo Ndejembi, na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Pololeti Mgema na Dk. Kedimon Mapana.

Ambapo Joel Makanyaga na Anderson Magolola walichukua fomu na kuzirudisha siku hiyo hiyo.

kwa upande wa Jimbo la Mtera ambalo lilikuwa linashikiliwa na Livingstone Lusinde, waliojitokeza kuchukua fomu walikuwa ni Mtoto wa Waziri mkuu mstaafu, John Malecela, Samweli Malecela, Lameck Lubote, Stephen Ulaya na Philip Elieza.

Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida wagombea wote waliofika kwenye ofisi za Wilaya za CCM kuchukua fomu walitumia mtindo wa Waziri wa Ujenzi ambaye alipitishwa na mkutano mkuu wa CCM kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho, Dk, John Magufuli kwa kuogopa kuonesha mbwembwe wakati wa kuchukua fomu kwa hofu ya kukatwa majina yao.

Wanachama wengi walikuwa wanachukua fomu kimya kimya na hata waandishi wa habari walipokuwa wakitaka kufanya nao mahojiano walikuwa wanaogopa kwa hofu ya kukatwa majina yao na vikao vya maamuzi vya chama hicho.