Ijumaa , 1st Jul , 2022

Watu watano wamefariki Dunia na wengine watano wamejeruhiwa katika ajali ya gari dogo, iliyotokea eneo la Lugulu Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Somanda Mjini Bariadi, Dk. Emmanuel Costantine, amesema katika majeruhi hao mmoja ni mtoto mwenye umri wa miaka miwili.

Tukio hilo la kusikitisha limehusisha gari dogo maarufu kwa jina la mchomoko T 789 DKM, lililokuwa limebeba abiria likitoka Wilaya ya Maswa kwenda Mjini Bariadi mkoani hapa

Dk. Emmanuel amesema katika majeruhi hao watano, wanne ni wa kiume na mmoja ni wa kike na miongoni mwa hao wa kiume mmoja ni mtoto wa miaka miwili. 

Amesema  hali ya majeruhi saizi (sasa hivi) inaendelea vizuri, miongoni mwao watatu walipata mshtuko wa ubongo lakini tayari wamezinduka na hali zao zinaendelea kuimarika

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda, amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa gari hilo, lililopinduka baada ya kugonga nguzo ya barabarani, wakati dereva wa gari hilo Seleman Masele (26) akimkwepa mwenda kwa miguu.

Kamanda Chatanda alipoulizwa na EATV iwapo dereva huyo wamemfanyia vipimo kujua endapo alikuwa ameelemewa na kilevi au mserereko wa dawa za kulevya, amesema bado hajafanyiwa vipimo kujua mambo hayo, hivyo hawezi kusema ndiyo au hapana.