Jumatano , 1st Dec , 2021

Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambanzi wamepoteza maisha katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, baada ya kutokea majibizano ya risasi baina ya polisi na watu hao, usiku wa kuamkia leo Desemba 01, 2021, majira ya saa 8:00 usiku.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Awadhi Haji

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Awadhi Haji, amesema kuwa polisi walipata taarifa za siri kuwa kuna kundi la watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameonekana katika milima ya Nyabugombe, Kata ya Nyakahura wilayani humo, na kwenda kukabiliana nao.

"Watu hawa walikuwa wanajiandaa kuteka magari na kufanya uporaji wa mali za watu katika eneo hilo, lakini kwa kuwa tulipata taarifa mapema tulifanikiwa kuwadhibiti kabla ya kutekeleza uhalifu," amesema Kamanda Awadhi.

Kamanda huyo amesema kuwa walipofika eneo la tukio waliwaona watu hao wakiwa wamevalia makoti marefu na kwamba walipowaamrisha kusimama ili wakaguliwe, ghafla walianza kuwarushia risasi polisi, nao wakaamua kujibu mapigo na kufanikiwa kuwajeruhi watu watatu na wanne wakafanikiwa kukimbia na eneo la tukio imepatikana bunduki moja aina ya AK 47 na risasi 51.