Jumanne , 22nd Sep , 2015

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi amesema kuwa watendaji wavivu katika manispaa nyingi na serikalini ndiyo chanzo cha migogoro mingi ya ardhi hapa nchini.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi

Lukuvi ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam alipokutana na wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam kusikiliza malalamiko yao ambapo wakazi wengi walijitokeza kuwasilisha malalamiko yao mbalimbali mbele ya waziri na ujumbe wake na kuahidiwa kutatua kero zao ndani ya miezi miwili.

Lukuvi ameongeza kuwa zoezi hilo ameagizwa kulifanya na Rais Jakaya Kikwete baada ya Rais kugundua kuwa watendaji wengi wa serikali na manispaa kushindwa kutatua migogoro mingi ya ardhi iliyo hapa nchini.

Aidha Lukuvi amesema kuwa mpaka sasa wizara yake imeshatatua migogoro 2500 kati ya migogoro 3180 katika mikoa zaidi ya mitano huku baadhi ya wenye madai wakisubiri kulipwa Fidia zao.