Ijumaa , 5th Aug , 2022

Watu zaidi ya 14 wameuawa na wengine 41 kujeruhiwa baada ya moto kuzuka katika ukumbi wa burudani Mkoa wa Chonburi uliopo kusini -Mashariki mwa Thailand.

Taarifa ya polisi imebainisha kuwa moto huo umezuka majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo katika klabu ya B nightspot katika wilaya ya Sattahip.

Kanda za video zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha watu wanaokimbia wakitoka ndani ya klabu huku  wakipiga mayowe, wengine nguo zao zikiwaka moto.

Ukumbi huko Chonburi, jimbo lililoko kilomita 150 kusini mwa Bangkok, lilikuwa jengo la ghorofa moja lenye ukubwa wa mita za mraba 4,800.

Wazima moto walipambana kwa zaidi ya saa mbili ili kudhibiti moto huo,  na baada ya kuuzima waliikuta miili ya watu waliopoteza maisha katika maeneo mbalimbali ya klabu hiyo.

Wengine walipatikana karibu na kibanda cha DJ. Kufikia sasa, wote waliofariki wanaaminika kuwa raia wa Thailand.