Alhamisi , 22nd Mei , 2014

Shule moja na nyumba zaidi ya 30 zimebomoka na kusababisha watu zaidi ya 190 kukosa makazi baada ya maporomoko ya udongo kutokea wilayani Ileje, mkoani Mbeya kutokana na mafuriko.

Moja ya nyumba zilizoathirika na mvua hizo

Shule moja na nyumba zaidi ya 30 zimebomoka na kusababisha watu zaidi ya 190 kukosa makazi baada ya maporomoko ya udongo kutokea katika vijiji vitatu wilayani Ileje, mkoani Mbeya ikiwa ni madhara yanayotokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha wilayani humo.

Mvua za masika ambazo zimenyesha kwa muda mrefu sasa wilayani Ileje zimesababisha mafuriko ya mto Sange na kutokea kwa maporomoko ya udongo ambayo yamebomoa shule na nyumba zaidi ya 30 za wananchi wa vijiji vya Sange, Lusalala na Luswisi, hali ambayo imesababisha kadhia kubwa kwa watu zaidi ya 190 kukosa mahali pa kuishi na hivyo kuiomba serikali, mashirika na watu binafsi kuwapatia misaada ya kibinadamu.

Mkuu wa wilaya ya Ileje, Rosemary Sitaki Senyamule ametembelea waathirika hao na kujionea athari za janga hilo kuelezea kusikitishwa kwake na madhara ambayo yamesababishwa na maporomoko hayo ya ardhi ndani ya wilaya yake.

Mvua za masika ambazo zimenyesha mwaka huu, zimesababisha madhara makubwa katika maeneo mbalimbali mkoani Mbeya, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu, mafuriko na maafa ya kwa binadamu.