Jumatano , 14th Jan , 2015

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania – TAKUKURU, leo imewafikisha katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, watumishi wawili waaandamizi wa umma kwa tuhuma za kuhusika na rushwa katika sakata la Escrow.

Watuhumiwa wakifikishwa mahakamani

Watuhumiwa hao ni pamoja na aliyekuwa Bw. Teophil John, ambaye ni Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini - REA, anayetuhumiwa kupokea fedha za Tanzania shilingi milioni 161.4 kutoka kwa mfanyabiashara Bw. James Rugemarila, fedha zinazodaiwa kuwa zilitolewa katika mazingira ya rushwa.

Mtuhumiwa mwingine ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Rugonzibwa Teophil ambaye kwa mujibu wa hati ya mashtaka, yeye anatuhumiwa kupokea fedha shilingi milioni 323, kutoka kwa Bw. Rugemarila pia katika mazingira yanayodhaniwa kuwa ni ya rushwa.

Katika kesi inayomkabili Bw. John, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Bw. Leonard Swai amedai mtuhumiwa akiwa kama mtumishi wa umma, alipokea fedha hizo kupitia akaunti aliyoifungua kwenye benki ya Mkombozi iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo Hakimu anayesimamia kesi hiyo, Frank Moshi, amemwachia mtuhumiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanye fedha za Tanzania shilingi milioni 25 kila mmoja.

Aidha, katika shtaka linamkabili Bw. Rugonzibwa, Hakimu Mfawidhi Bw. Emilius Mchauru amemtaka mtuhumiwa huyo kuwa na mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha pesa alichokipokea, pamoja na wadhamini wawili ambao kila mmoja atawasilisha mahakamani hapo fedha za Tanzania shilingi milioni kumi.

Watuhumiwa wote wametimiza masharti na sasa wapo nje kwa dhamana ambapo kesi inayomkabili John itatajwa tena Januari 29 mwaka huu wakati Rugonzibwa ametakiwa afike mahakamani hapo keshokutwa Ijumaa ambapo kesi yake itatajwa tena pamoja na kupitia kuona iwapo vielelezo vya dhamana vinakidhi mahitaji ya mahakama.