Waziri Dk. Mpango alivyotoa chozi leo

Jumanne , 23rd Feb , 2021

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango, leo ametoa machozi wakati akikumbuka ndugu, rafiki na viongozi wenzake waliotangulia mbele za haki akiwemo Mhandisi Atashasta Nditiye na Prof. Benno Ndulu pamoja na Balozi John Kijazi.

Waziri wa Fedha na Mipango (katikati), Dkt. Philip Mpango,na pembeni yake ni madaktari wa hospitali ya Benjamin Mkapa waliokuwa wakimhudumia

Hayo yamejiri hii leo Februari 23, 2021, Jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya madaktari wa hospitali ya Benjamin Mkapa, kujiridhisha kwamba afya yake imeimarika na anaweza kuendelea na majukumu ya kulijenga taifa.

"Nimekaa hapa nikihudumiwa na hapa peke yake ni zaidi ya siku 10 na nilikuja na mtungi kabisa wa Oksijeni na leo ni siku ya tatu sijagusa kabisa mtungi wa Oksijeni kwa kweli nataka niwaambie Watanzania afya yangu imeimarika,” alisema Waziri Dk. Mpango.

Aidha Waziri Dk. Mpango ameongeza kuwa "Acheni Mungu aitwe Mungu tuendelee kumtukuza na kumuomba yeye ndio muweza wa yote namshukuru sana kwa huruma yake najua ananipa nafasi ya kuendelea kuitumikia nchi kwa nafasi ya pekee sana napenda kumshukuru Rais Dk. John Magufuli na familia yake nitasema tu ukweli hakuna siku ambayo Mh. Rais hakunipigia simu si mara moja si mara mbili".