Jumatano , 8th Jun , 2016

Zile tetesi za kukamatwa kwa mwanamuziki nguli wa tungo zenye ujumbe Vitalis Maembe, zimepigiwa mstari na Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi.

Akiongea na Planet Bongo ya East Africa Radio leo, Kamanda Mushongi amethibitisha kukamatwa na mwanamuziki huyo, na kwamba ameshafikishwa mahakamani, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutotii amri ya polisi wakati wa maandamano ya wanafunzi katika chuo cha sanaa Bagamoyo.

“Kulikuwa kuna tatizo pale chuo cha sanaa Bagamoyo, kulikuwa kuna vurugu za wanachuo kwamba kukataa mitihani, wenyewe walikuwa wanataka kwamba chuo cha sanaa watoe mitihani ambayo iwe inatambulika na VETA, lakini wenyewe kama chuo wanasema wana mitihani yao, sasa kwa hiyo kuna vurugu za sintofahamu, ikabidi polisi iende pale, iliwakamata wanafunzi na kuwaleta kituo cha polisi.

Kamanda Mushongi aliendelea kuelezea ….............Yeye (Vitalis Maembe) alienda kule nasikia ana wanafunzi wake pale, akalazimisha kuingia ndani, kuitwa na polisi njoo utoke yeye hataki kutoka, tumeshampeleka mahakamani tu ndo dawa, hii mambo ya dhamana inasumbua”, alisema Kamanda Mushongi.

Pamoja na hayo Planet Bongo ilizungumza na Rose ambaye ni mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, na kuelezea jinsi ilivyokuwa siku ya tukio.

Sauti ya Mwanafunzi Rose akielezea jinsi tukio lilivyokuwa na kukamatwa kwa Vitalis Maembe
Sauti ya Kamanda Mushongi akielezea kukamatwa kwa Vitalis Maembe