Jumamosi , 11th Jun , 2016

Kocha Mkuu wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Shaibu Amodu amefariki dunia akiwa ana umri wa miaka 58 kifo hicho cha ghafla ni kama kutonesha kidonda cha mashabiki wa soka nchini humo ambao siku chache zilizopita waliondokewa na kocha Keshi.

Kocha Mkuu wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Marehemu Shaibu Amodu.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFF), Amodu amefariki leo Jumamosi Benin City baada ya kulala salama na kushindwa kuamka.

Kocha huyo wa zamani wa BCC Lions, inafahamika alikuwa analalamikia maumivu ya kifua kabla ya kwenda kulala usiku wa jana.

"Hiyo ni sahihi," amesema Katibu Mkuu wa NFF, Dk Mohammed Sanusi, akithibitisha kifo cha Amodu. "Alilala na hakuweza kuamka,"amesema.

Msiba huu unatokea wakati Wanigeria bado wapo katika msiba mwingine wa gwiji wake mwingine Stephen Keshi, mchezaji na kocha wa zamani wa Super Eagles aliyefariki dunia pia Benin City Jumatano.

Amodu na Keshi walifanya kazi pamoja Nigeria kama Kocha Mkuu na Msaidizi wake katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2002 nchini Mali.

Novemba 1994, Amodu aliiongoza kwa mara ya kwanza Super Eagles katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa ikifungwa 1-0 na England.

Aliiongoza Super Eagles katika awamu nne tofauti kuanzia 1994 na 1995 na 1997, 2001 na 2002 na kati ya 2008 na 2010.

Amodu anakumbukwa kwa kuiwezesha BCC Lions kutwaa Kombe la Washindi Afrika mwaka 1990 (sasa Kombe la Shirikisho) na pia kuifikisha Super Eagles Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002

Hadi anakutwa na umauti, Amodu alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa NFF.

Siku chache baada ya kifo cha Stephen Keshi aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taiga ya Nigeria, kocha mwingine wa timu hiyo maarufu kama Super Eagles, Shaibu Amodu naye amefariki dunia, leo.