Baada ya miaka 8 Man United yaonja mafanikio

Jumatano , 13th Jan , 2021

Klabu ya soka ya Manchester United ya nchini England, imeibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Burnley kwenye mchezo wa ligi kuu nchini humo uliopigwa usiku wa kuamkia leo Januari 13, 2021.

Paul Pogba akishangilia goli na wenzake

Baada ya ushindi huo ambao goli pekee lilifungwa na Paul Pogba dakika ya 71, Manchester United sasa imefikisha pointi 37 na kukaa juu ya  msimamo ikiwazidi Liverpool ambao wana pointi 33, baada ya timu zote mbili kucheza mechi 17 mpaka sasa.

Hii ni mara ya kwanza Manchester United inaongoza ligi kuu ya England baada ya kuwa imecheza mechi nyingi (17), ambapo mara ya mwisho kuongoza ligi baada ya mechi nyingi ilikuwa ni siku ya mwisho ya msimu wa 2012-13 walipotwaa ubingwa chini ya Sir Alex Ferguson.

Wachezaji wa Manchester United wakishangilia goli

Hata hivyo mbio za ubingwa ndio kwana mbichi kutokana na ushindani ambao upo msimu huu ambapo vilabu vingi vimekuwa vikisuasua.

Katika ligi ya msimu huu nchini England  karibu timu sita zimeshakaa kwenye usukani wa ligi ya nchi hio mpaka sasa ambazo ni  Manchester United, Southampton, Aston Villa, Liverpool, Tottenham na Everton.