Alhamisi , 13th Jan , 2022

Miamba ya soka nchini Uhispania, FC Barcelona imetolewa kwenye hatua ya Nusu fainali ya Spanish Super Cup baada ya kufungwa mabao 2-1 ddhidi ya Mahasimu wao Real Madrid usiku wa jana nchini Saudi Arabia.

(Federico Valverde wa Madrid akishangilia baada ya kufunga bao la ushindi)

Real Madrid walikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa winga wake kinda, Vinicius JR dakika 25 kabla ya Luuk De Jong kuisawazishia Barcelona dakika ya 41 na timu kwenda mapumziko kwa sare ya 1-1.

Karim Benzema aliwapa tena Uongozi Madrid kwa kufunga bao dakika ya 72 na kudhani wameshatinga fainali, lakini Ansu Fati aliisawazishia tena Barcelona akitokea benchi dakika ya 83 na kufanya mchezo kuongezwa dakika 30.

Shujaa wa mchezo huo aliibuka kuwa, Kiungo Federico Valverde aliyefunga bao dakika 98 na kuwachoma Barcelona kisu kikali kwenye  mfupa na kuzidi kuwapa wakati mgumu.

Mchezo ulimalizika kwa Real Madrid kutinga fainali ya Spanish Super Cup inayoendelea nchini Saudi Arabia huku akisubiri mshindi kati ya mchezo wa Athletic Bilbao dhidi ya Atletico Madrid utakaochezwa sasa 4:00 usiku wa leo huku fainali ikitazamiwa kuchezwa Januari 16, 2022.