Alhamisi , 2nd Dec , 2021

Kocha wa muda wa Manchester United, Michael Carrick amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuacha kumdhihaki Ronaldo kwamba hataweza kucheza kwenye mfumo mpya wa mwalimu wa mpito wa United Ralf Rangnick.

(CR7 akiwa anapokea maelekezo kutoka kwa kocha wake Michael Carrick)

Rangnick, Raia wa Ujerumani anasifika kwa kutumia mfumo wa uchezaji maarufu kama 'gegenpressing' ambao hulazimisha wachezaji wanapopoteza mpira kukaba kwa nguvu na haraka kupokonya mpira kwa wapinzani na kushambulia kwa haraka kitu ambacho mashabiki wengi wanaona  Ronaldo 36, hataweza kuingia  kwenye mfumo huo kutokana na kasi na umri wake kumtupa mkono.

"labda ni hadithi tu kwamba Ronaldo haweza kucheza mfumo huo, amecheza  kwa muda mrefu kwenye timu nyingi  na amefanikiwa kucheza kwenye mifumo tofauti tena kwa mafanikio makubwa ”  Amesema Carrick.

Kwenye mchezo dhidi ya Chelsea Michael Carrick alimuweka benchi Ronaldo ambaye ndiye kinara wa magoli ndani ya United akifunga magoli 10 katika michezo 15 ya mashindano yote waliyocheza mpaka  sasa.

Manchester United saa 5:15 usiku leo watakuwa Old Trafford kuwakabili Arsenal ambapo Cristiano Ronaldo ana rekodi ya kufunga magoli sita kati ya michezo 15 aliyokutana na washika bunduki wa Emirates, Arsenal.