Jumanne , 21st Sep , 2021

Afisa Mtendaji Mkuu wa bodi ya ligi kuu ya Tanzania bara, Almas Kasongo amesema kuwa maandalizi kuelekea mchezo wa Ngao ya jamii kati ya Simba na Yanga, yanaendelea vizuri huku TPLB, ikiendelea kushirikiana na wadau wa kandanda nchini ili kuondoa dosari zinazojitokezaga.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo akiongea kuhusu waamuzi mbele ya Wanahabari.

Kasongo amesema kuwa changamoto mbali mbali ikiwemo za tiketi, wameendelea kuzishughulikia pamoja na zile zilizojitokeza kipindi cha matamasha ya Wiki ya Mwananchi na lile la Simba Day, na iwapo zitajitokeza tena siku ya septemba 25, ziwe mpya na sio za zamani.

Bodi ya ligi imendelea kutoa semina nyingi za kujengeana uwezo kwa wadau wote wa michezo, ikiwemo kwa wanahabari, maafisa habari wa vilabu pamoja na mameneja.

Pia Kuelekea katika mtanange wa Ngao ya jamii, bodi ya ligi imeelekeza nguvu zaidi kwa waamuzi wa mchezo huo, ilikuondokana na makosa na lawama za mashabiki kutokana na udhaifu wa kutafsiri sheria 17 za kabumbu. 

Simba na Yanga zitachuana siku ya Jumamosi kuashiria ufunguzi wa ligi kuu Tanzania bara kwa msimu wa mwaka 2021/2022.