Alhamisi , 1st Dec , 2022

Serikali imepongeza Chama cha Mchezo wa Judo nchini kwa utendaji bora ambao ndani ya muda mfupi kimefanya mabadiliko makubwa ya utendaji ambapo imeahidi mchezo huo kupatiwa vyumba vya kuchezea katika viwanja vya michezo nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu Said Yakub wakati akizungumza ofisini kwake Mtumba Dodoma na Rais wa Mchezo wa Judo Nchini ndugu Zaidi Hamisi.

“Mmeainisha mambo mengi ya muda mfupi na ya muda mrefu, jambo la msingi chama cha Judo lazima kiwe taasisi kamili, yenye mipango ya muda mrefu, muwe na mpango mkakati wa miaka mitano, muwe na kituo cha mafunzo, hapo litakuwa eneo ambalo mafunzo ya mchezo huo yatafanyika" amesema Said Yakubu.

Naibu Katibu Mkuu Yakubu amesema, Serikali itaratibu ufundishaji wa Judo shuleni kwa ushirikiano na wizara zinazosimamia shule, huku akimshukuru Rais wa Shirikisho la Judo Ulimwenguni Ndugu Marlus Vizer kwa kutoa msaada wake kwa michezo huo na kusema wamemualika aje Tanzania kukutana na viongozi wa mchezo huo nchini.

Kwa upande wake Rais wa Mchezo wa huo, Ndugu Hamisi amepokea pongezi hizo na kusema kuwa, Tanzania itapokea jozi 50 ya nguo za mchezo wa judo katika mashindano ya kimataifa, jozi 100 za nguo za mafunzo ya mchezo huo na pia jozi 200 za nguo za mazoezi kwa ajili ya wanafunzi na pia Tanzania itapata nafasi ya kusomeshewa walimu wa mchezo huo kwa ngazi ya shahada.

Judo ni mchezo wenye asili ya Japan huku ukichezwa sana katika mataifa ya Bara Ulaya ikiwamo Ufaransa.