Ijumaa , 3rd Jun , 2016

Bondia Mtanzania Cosmas Cheka kesho anapanda ulingoni Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam kupambana na bondia kutoka nchini Malawi, Chrispin Moliyati katika pambano la kuwania ubingwa wa Universal Boxing Union (UBO) wa uzito wa Super Feather.

Cosmas Cheka akivishwa mkanda wa WBF alioutwa hivi karibuni.

Pambano hilo la raundi 12 limeandaliwa kwa lengo la kuendeleza mchezo wa ngumi za kulipwa nchini na litasaidia kwa bondia huyo kumpandisha kiwango chake ili aweze kucheza mapambano makubwa duniani.

Cheka ambaye ni mdogo wa bondia bingwa wa dunia wa WBF Francis Cheka [SMG] amesema kuwa amejiandaa vyema kwa pambano hilo na anataka kuonyesha ubora wake katika mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.

Cheka amesema kuwa anatarajia kushinda katika pambano hilo ili kuendeleza rekodi yake katika ngumi za kulipwa.

“Moliyati ni bondia mzuri na najua atanipa upinzani mkali, lakini sitakubali kupoteza katika ardhi ya Tanzania, nimejiandaa vizuri kwa ajili ya pambano hilo,”.

Mbali ya mapambano hayo, pia kutakuwa na ‘mawe’ ya aina yake katika mapambano ya utangulizi.

Bondia nyota, Japhet Kaseba atawania ubingwa wa Taifa wa TPBC Limited dhidi ya bondia nyota kutoka Zanzibar, Amour Mzungu katika pambano la uzito wa juu.

Pia Alphonce Mchumiatumbo atazipiga na bondia Mussa Ajibu kutoka Malawi katika pambano la uzito wa juu kabla ya Ashraf Suleiman kuonyeshana kazi na Aliki Gogodo wa Malawi katika pambano la uzito wa juu pia.

Pambano lingine la ubingwa litakuwa kati ya bondia Shabani Kaoneka dhidi ya Zumba Kukwe la uzito wa middle raundi 10 ambapo Yonas Segu atazichapa na bondia wa Malawi, Wilson Masamba katika pambano la uzito wa Light-Welter la raundi nane.

Mabondia wa kike, Lulu Kayage atazichapa na Enelesi Nkwanthi katika pambano la uzito wa bantam la raundi sita.