Alhamisi , 13th Jan , 2022

Matajiri wa Jiji la London, Klabu ya Chelsea imefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Carabao msimu wa mwaka 2021-22 baada ya kuifunga Tottenham Hotspurs 1-0 usiku wa jana kwenye mchezo wa mkondo wapili wa Nusu Fainali.

(Rudiger akifunga bao kwa kichwa na kuipa Chelsea ushindi wa 1-0 )

Bao pekee la ushindi wa Chelsea limefungwa na beki wake kitasa, Antonio Rudiger na kufanya Chelsea ishinde kwa magoli 3-0 katika michezo miwili ya Nusu fainali hiyo baada ya ushindi wa mabao 2-0 kwenye Nusu fainali ya kwanza

Kutinga huko fainali, Chelsea wameweka rekodi ya kibabe ya kitinga fainali tatu katika muda wa mwaka mmoja atokea kocha Thomas Tuchel ajiunge nayo Januari 2021.

Fainali ambazo Chelsea wametinga chini ya Tuchel ni ile ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ambaye walikuwa Mabingwa mbele ya Manchester City, Kombe la FA waliopoteza kwa Leicester City na sasa Kombe la Carabao.

Ushindi huo pia ni Matumaini mapya kwa Chelsea ambao hawajatinga fainali ya kombe hilo kwa miaka mitatu iliyopita huku wakiwa hawajabeba ubingwa huo kwa miaka saba iliyopita.

Chelsea atacheza fainali dhidi ya mshindi kati ya Arsenal na Liverpool ambao mchezo wao utachezwa saa4:00 usiku wa leo kabla ya kurudiana Januari 20, 2022 na Fainali kutaraji kuchezwa Februari 27, 2022.