Jumatano , 24th Dec , 2014

Timu ya Coastal Union inatarajia kuelekea jijini Mbeya hapo kesho kwa ajili ya mechi ya Ligi kuu Tanzania Bara wanayotarajia kucheza na timu ya Tanzania Prisons Desemba 26, uwanja wa Sokoine mjini humo.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa Coastal Union, Oscar Assenga amesema kuwa anaamini kikosi cha timu hiyo kilicho chini ya kocha James Nandwa kitafanya vizuri.

Assenga amesema timu hiyo inaondoka ikiwa na wachezaji pungufu kutokana na kuwa na majeruhi wawili ambao ni Keneth Masumbuko na Yayo Kato Lutimba ambao waliumia mazoezini lakini anaamini wachezaji waliobakia wataweza kuvuna pointi tatu muhimu za ugenini.

Assenga amesema timu hiyo imecheza mechi mbalimbali za kirafiki na kocha ameweza kujua mapungufu yaliyopo katika kikosi hicho na ameweza kuyafanyia kazi hivyo anaamini timu hiyo itafanya vizuri katika mechi zote zilizobakia.

Assenga amesema Klabu hiyo hivi sasa inajikita zaidi katika kuangalia vipaji vya vijana walio katika kikosi cha pili ambao wanaamini wana uwezo mzuri kama wakiwasimamia watafanya vizuri ili kuweza kusaidia kikosi cha Kwanza.