Jumanne , 17th Mei , 2016

Baada ya kuanda michuano ya vijana Afrika Mashariki uongozi wa Riadha Tanzania (RT) umesema jiji la Dar es Salaam litakuwa mwenyeji kwa mara nyingine wa mashindano makubwa ya riadha lakini safari hii ni ya taifa yatakayoshirikisha mikoa yote nchini.

Baadhi ya wanaridha wakichuana katika moja ya mashindano ya taifa.

Zaidi ya wanariadha 345 na viongozi wao zaidi ya 44 kutoka mikoa mikoa yote hapa nchini Tanzania bara na visiwani wanataraji kushiriki mashindano ya taifa ya riadha itakayofanyika jijini Dar es Salaam katika uwanja wa taifa kuanzia Juni 3 nakumalizika Juni 4 mwaka huu.

Akizungumzia maandalizi ya michuano hiyo Kaimu Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania RT Omben Zavara amesema taratibu zote za kiitifaki na maandalizi zimezingatiwa na kukamilika tayari kwa michuano hiyo itakayoshirikisha mbio zote kuanzia fupi za mita 100 na zile ndefu zaidi za mita 10,000 huku pia washiriki wakionyeshana umwamba katika michezo ya miruko ya juu na chini na mitupo ya mikuki na visahani.

Aidh,a Zavara ambaye aliwahi kuwa bingwa wa kimataifa wa mbio ndefu kwa upande wa wanawake miaka ya nyuma enzi za kina Bayi, Ikangaa na Nyambui ameitaka mikoa kufanya maandalizi mazuri kwa wanaridha wao ili kuleta ushindani na kupata wanariadha bora wa taifa watakaokimbia muda mzuri wa kimataifa na kuwa tayari kuiwakilisha nchini katika medani ya kimataifa.

Amesema itakuwa jambo la ajabu na watachukuwa hatua kali sana ikiwemo kuutoa mashindanoni mkoa wowote utakaokuja bila wanaridha wa mkoa wake na kuamua kuokota ama kukusanya wanaridha wa Dar es Salaam nakuwafanya kama timu ya mkoa wao ili kushiriki michuano hiyo.

Akimalizia Zavara ametowa wito kwa wadau wa michezo kote nchini, makampuni na serikali kwa ujumla kuisaidia RT kuboresha mashindano hayo kwa kudhamini maandalizi na zawadi kwa washiriki kwa lengo la kuwapa motisha washiriki ili waweze kufanya vema katika michuano hiyo.

Zavara amesema udhamini huo pia utalenga kusaidia vifaa kwa washiriki lakini pia wao RT kama wasimamizi wakuu kuweza kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji wa mashindano hayo ya siku mbili.

Pia amemalizia kwakutoa wito kwa mashabiki wa michezo kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa taifa kwa siku zote mbili ili kushuhudia wanariadha kutoka maeneo ya alisi zao wanavyopambana kushindania mikoa yao.