Jumatatu , 16th Sep , 2019

Droo ya hatua ya nusu fainali ya michuano ya Sprite Bball Kings 2019 imefanyika leo katika ofisi za EATV na EA Radio, ambapo vigogo wanne waliofuzu hatua hiyo wamepangwa katika mechi mbili.

Droo ya nusu fainali ya Sprite Bball Kings 2019

Timu zilizofuzu hatua ya nusu fainali ni KG Dallas, Flying Dribblers, Tamaduni na Mchenga Bball Stars ambapo kwenye hatua yenyewe ya nusu fainali, timu ya Flying Dribblers imepangwa na Mchenga Bball Stars huku KG Dallas ikipangwa na Tamaduni.

Kabla ya droo hiyo, baadhi ya wawakilishi wa timu za nusu fainali walitoa maoni yao, wa kwanza ni mwakilishi wa Tamaduni, Denis Babu ambaye alisema, "msimu huu tumejipanga zaidi ya mwaka jana, sisi tunataka hela tuu hatujali mtu yoyote hata kama droo isipochezeshwa, tangazeni tuu. Hawa Mchenga wataitwa mchanga tu".

Baada ya droo kupangwa, mwakilishi wa Flying Dribblers ambaye timu yake imepangwa na bingwa mtetezi Mchenga Bball Stars, amesema kuwa uzoefu umewasaidia sana kufika hapo na hawatofanya makosa kama msimu wa kwanza ambao walitolewa katika nusu fainali na mabingwa hao mara tatu mfululizo.

Michezo ya nusu fainali inatarajiwa kuwa mitatu ( best of three ), ambapo mchezo wa kwanza unatarajia kupigwa Jumamosi Septemba 21 katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, mchezo wa pili utapigwa Jumatano Septemba 25. Eandapo washindi hawatapatikana katika 'best of two' mchezo wa tatu utapigwa Jumamosi Septemba 28.