Jumatatu , 5th Dec , 2022

Kiungo Feisal Salum amewaondoa presha mashabiki wa Yanga na kuwaomba waendelee kuiombea timu yao kwenye mbio za Ubingwa msimu huu.

Feisal aliyefunga bao pekee, Wananchi tukishinda 1-0 mbele ya Prison, amekiri kuwa Ligi msimu huu ni ngumu kutokana na ratiba kuwa na mechi za karibu mfululizo lakini kwa nguvu za mashabiki, wao watapambana kuhakikisha Yanga inatetea ubingwa wake.

“Ligi msimu huu ni ngumu sana. Mbali na wapinzani kuimarika zaidi, ratiba pia imekuwa ikitubana sana.

“Sisi wachezaji tunatambua jukumu letu ni kupambana kuhakikisha timu yetu inatetea ubingwa, hivyo niwaombe mashabiki wa Yanga kuendelea kutuombea na kuisapoti timu yao katika kipindi hiki,” amesema  Feisal.

Yanga itashuka kwenye uwanja wa Majaliwa, siku ya Jumatano kuvaana na Namungo FC ukiwa ni mchezo wa kiporo kwa Yanga kukamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC.