Ijumaa , 16th Aug , 2019

Msanii wa kundi la Weusi, Gnako 'Warawara', leo amefunguka kitu kinachomvutia kwenye msimu huu wa mashindano ya Sprite Bball King's ambayo yameandaliwa na East Africa Television na East Africa Radio kwa kushirikiana na kinywaji cha Sprite.

Msanii wa Weusi, Gnako

Akizungumza na  EATV & EA Radio Digital, Gnako amesema amefarijika na maandalizi ya msimu huu na yeye ni miongoni mwa wafuatiliaji wazuri wa mchezo wa mpira wa kikapu na amehudhuria mechi nyingi za mchezo huo lakini ameeleza masikitiko yake juu ya kutelekezwa kwa vipaji vinavyozalishwa.

"Nafuatilia sana mchezo wa 'Basketball', nilishapata bahati ya kwenda kwenye mashindano navutiwa kuona kama kuna vipaji, isipokuwa kinachoniumiza baadaye vile vipaji vinakuwa havina muendelezo baada ya kufanyika mashindano", amesema Gnako.

Aidha msanii huyo ameendelea kueleza kwamba "nafikiri kitu kizuri kiwepo baada ya mashindano ya Sprite Bball Kings,  bora kungekuwa na ligi au vitu ambavyo vinakuwa vinaendelea kutokea baada ya mashindano kwa sababu vipaji vikishapatikana vinakuwa vinaeleaelea". 

Ufunguzi wa mashindano hayo utafanyika kesho Jumamosi katika viwanja vya Mlimani City, Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine kutakuwa na usajili wa timu shiriki katika michuano hiyo. Kamati ya mashindano inazialika timu zote nchini kuja kujiandikisha ambapo umri wa wachezaji ni kuazia miaka 16 na kila timu itaruhusiwa kuwa na wachezaji 10.