Jumatatu , 19th Aug , 2019

Baada ya michuano ya Sprite Bball Kings 2019 kuzinduliwa hapo jana katika viwanja vya Mlimani City, ratiba ya hatua ya mtoano ya michuano hiyo itaanza Jumapili ya wiki hii, Agosti 25 katika kituo cha michezo cha JK Park, Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 Asubuhi.

Moja ya picha katika uzinduzi wa Sprite Bball Kings 2019

Michuano hiyo inayoandaliwa na East Africa TV na East Africa Radio kwa kushirikiana na kinywaji cha Sprite, itaanzia hatua ya mtoano ambayo itahusisha timu zote zilizojisajili kwa msimu huu isipokuwa mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars, ambayo itaanzia katika hatua ya 16 bora. 

Mpaka sasa zaidi ya timu 40 zimejisajili kushiriki michuano hiyo na zingine zikiendelea kuongezeka, ambapo Agosti 21 timu zote zitafanyiwa semina 'Workshop' ili kufahamu sheria za mashindano, vigezo pamoja na kukabidhiwa vifaa muhimu. Semina hiyo itafanyika katika ofisi za EATV na EA Radio, zilizopo Mikocheni Dar es Salaam.

Pia zoezi la usajili bado linaendelea leo Jumatatu, Agosti 19 na Jumanne, Agosti 20 kwa wawakilishi wa timu husika kufika katika ofisi za EATV na EA Radio, Mikocheni Jijini Dar es Salaam.