Ijumaa , 1st Apr , 2016

Baada ya danadana za takribani wiki mbili hatimaye kesho mzizi wa fitna wa maamuzi ya kamati ya nidhamu ya TFF utakatwa kesho na mashabiki kujua ni nini kimejili katika sakata la upangaji matokeo ya michezo ya mwisho ligi daraja la kwanza FDL.

Kikosi cha timu ya Geita Gold Sports ya Geita.

Kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kitaendelea kesho Jumamosi saa 3 asubuhi katika ofisi za TFF zilizopo Karume, na maamuzi yake yatatangazwa saa 7 mchana.

Kamati inakutana kwa ajili ya kumalizia shauri la upangaji wa matokeo Ligi Daraja la Kwanza (StarTimes League) kundi C inayozihusisha timu za Geita Gold, JKT Kanembwa, JKT Oljoro na Polisi Tabora.

Viongozi watakaohojiwa na Kamati ya Nidhamu ni, Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tabora), Fateh Remtullah (Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tabaora), viongozi wa benchi la ufundi Polisi Tabora, Mrisho Selemani, Boniface Komba, Bernard Rabiamu.

Kamati pia itawahoji Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita, Salum Kurunge na mwenyekiti wa Klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita.

Ikumbukwe JKT Kanembwa ilifungwa mabao 8-0 na Geita Gold SC katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Polisi Tabora ilishinda mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Baada ya hapo, TFF ilitangaza kusitisha matokeo hayo na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi (Kamati ya Saa 72) iliyokutana Februari 16, mwaka huu kupitia taarifa za mechi hizo mbili ikalipeleka suala hilo Kamati ya Nidhamu kufuatia kutilia mashaka upangaji wa matokeo.