Ijumaa , 21st Jan , 2022

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amemsifu mshambuliaji wake Diogo Jota kwa kiwango bora baada ya kufunga mabao 2 kwenye ushindi wa 2-0 walioupata kwenye mchezo wa nusu fainali ya kombe la Ligi Carabao CUP dhidi ya Arsenal. Na sasa watacheza fainali dhidi ya Chelsea.

Diogo Jota kushoto akipongezwa na kocha Jurgen Kloop

Ushindi huo wa mabao 2-0 ulitosha kuifanya Liverpool kukata tiketi ya kucheza fainali ya Carabao Cup na ulikuwa ni mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya michuano hiyo mabao yote mawili ya Liverpool yamefungwa na Diogo Jota dakika ya 19 na 77. Na sasa Liverpool wataminyana na Chelsea katika mchezo wa fainali Februari 27, 2022.

Mara baada ya mchezo huo kocha wa Liverpool Mjerumani Jurgen klopp akasifu kiwango bora cha Jota na umuhimu wa magoli aliyofunga jana hususani kipindi hiki ambacho Mo Salah na Sadio Mane hawapo kwenye kikosi.

"Wow, yupo kwenye kiwango bora,Tuliamini alipofika kwenye klabu atatusaidia kwa kiasi kikubwa. Mawazo yake na ubora wake ndivyo vilivyotufanya kumsajili.Tangu alivyojiunga nasi amepiga hatua, amekuwa mshambuliaji wa kiwango cha Dunia. Amesema Klopp.

Jota kafikisha mabao 14 kwenye michuano katika michezo 27 msimu huu, Lakini pia amefunga jumla ya mabao 27 katika michezo 57 tangu alipojiunga na klabu hiyo msimu uliopita wa 2020-21. Liverpool imekata tiketi ya kucheza fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0 kwenye michezo ya mikondo miwili ya nusu fainali mchezo wa mkondo wa kwanza ulimalizika kwa suluhu 0-0 katika Dimba la Anfield.