Jumamosi , 18th Jun , 2016

Wanachama, Mashabiki na Wapenzi wa klabu ya Yanga kwa namna tofauti wameendelea kuiombea dua timu hiyo ambayo leo usiku inataraji kushuka dimbani nchini Algeria kucheza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano ya kombe la shirikisho Afrika.

Kikosi cha timu ya soka ya Yanga.

Yanga leo inatarajiwa kucheza na MO Bejaia ya Algeria ikiwa ni mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mchezo huo ukichezwa kwenye Uwanja wa l’Unite Maghrebine uliopo Bejaia, nchini Algeria.

Wakizungumza hii leo mashabiki wa timu hiyo kutoka matawi mbalimbali jijini Dar es Salaam kila mmoja amekuwa akiomba dula lake kuitakia timu hiyo mafanikio ya ushindi katika mchezo utakapigwa usiku wa saa sita na robo kwa muda wa saa za Afrika Mashariki.

Mashabiki wa timu hiyo ya Yanga wanautazama mchezo huo kwa jicho tofauti kwanza wakizungumzia figisufigisu za waarabu wa Afrika hasa wanapocheza na timu za kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambapo wanakuwa na vituko vingi vya kusaka ushindi kwa njia zisizofaa nje ya uwanja kwa kuwavuruga wapinzani nje na ndani ya uwanja.

Aidha, Mashabiki hao waliokuwa wanajiamini kwa asilimia 100 wamekiri ugumu wa mchezo huo lakini wakiwa na uhakika wa kupata matokeo chanya katika mchezo huo kama si kushinda basi hata matokeo ya sare na si kufungwa jambo ambalo wamesema kimsingi safari hii halitotokea kamwe hasa kutokana na ubora wa kikosi hicho na pia uzoefu ambao tayari wameupata wakucheza na timu za kiarabu na hii ni baada ya kufanikiwa kuidhibiti Al Ahly ya huko Misri ambayo ilipata ushindia wa taabu ikiwa nyumbani jambo ambalo sasa wanayanga hao wamesema ni historia.

Kikosi cha Yanga ambao ni mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara na mabingwa wa kombe la Shirikisho kilishatua nchini humo [Algeria] kikitokea nchini Uturuki amako walikuwa na kambi maalumu ya maadnalizi ya michuan hiyo ya CAF wakijichimbia katika mji maarufu sana wa Antalia na tayari hivi sasa kikosi kamili cha timu hiyo kipo gado katika mji wa Bejaia.

Pamoja na kuwakosa nyota wake wawili katika nafasi ya ulinzi kama beki wa kulia Juma Abdul ambaye ni majeruhi na beki wa kati Nadir Haroub maarufu kama Cannavaro bado wanachama wa timu ya Yanga wanaimani na kikosi hicho ambacho kimetimia kila idara msimu huu huku pia kikipata nguvu mpya baada ya kuongezewa nguvu mpya tano wakati huu wa dirisha la usajili lililofunguliwa juzi Juni 15 mwaka huu.

Yanga pamoja na kumkosa beki wake wa kulia Juma Abdul ambaye tayari uhenda nafasi yake ikazibwa na chipukizi mwenye kasi beki Hassani Ramadhan Kessy waliyemnyakuwa kutoka Simba kama taratibu za CAF zikikamilika pia itamkoasa beki wa kati Cannavaro ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola.

Katika nafasi hiyo wanachama hao wamesema hawana shaka yoyote kwani imesheheni vilivyo na hii ni kutokana na uwepo wa beki kisiki chipukizi waliyemsainisha kutoka kwa wakata mwiwa wa Manungu Turiani Mkoa wa Morogoro timu ya Mtibwa Sukari Vincent Andrew maarufu kama Dante lakini pia ukimwondoa kiraka Mnyarwanda Mbuyu Twite nafasi hiyo huwa inazibwa na beki mrefu mwenye misuli raia wa Togo mwenye asili ya Ivory Coast Vicent Bossou ambaye hucheza nafasi hiyo pamoja na beki huyo mahiri wa mipira ya kichwa kutofanya mazoezi kikamilifu na wenzake kutokana na kuchelewa kujiunga nao lakini anauhakika wa kuanza kutokana na uzoefu wake katika michuano mikubwa ya kimataifa.

Katika kukiimarisha kikosi cha timu hiyo Yanga mbali na usajili wa beki Andrew Vicent 'Dante', hadi sasa Yanga imewasajili Hassan Kessy kutoka Simba ya Dar es Salaam, Juma Mahadhi (Coastal Union) ya Tanga na Beno Kakolanya kutoka Prisons Mbeya.

Wakati huo huo mara baada ya klabu ya Yanga kukamilisha usajili wa rekodi na kutuma jina CAF la mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa, kiungo huyo mshambuliaji amendoka alfajiri ya jana kwenda Algeria kuungana na timu yake mpya, ikiwani baada ya kutia saini Mkataba wa miaka miwili.

Chirwa aliwasili jioni ya jana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na muda mfupi baadaye akasaini Mkataba wa miaka miwili.

Na mara moja Yanga ilituma jina lake makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika siku ya mwisho ya usajili mdogo wa mashindano ya Afrika na sasa Yanga wanatarajia kupata leseni yake na CAF kuanzia leo jioni ili kukamilisha idadi ya wachezaji watano wapya, baada ya wazawa kipa Benno Kakolanya kutoka Tanzania Prisons ya Mbeya, mabeki Hassan Kessy wa Simba , Andrew Vincent Mtibwa na kiungo Juma Mahadhi kutoka Coastal Union ya Tanga.