Jumamosi , 17th Aug , 2019

Michuano ya Sprite Bball Kings 2019 inayoandaliwa na EATV, EA Radio kwa kushirikiana na kinywaji cha Sprite imezinduliwa Jumamosi Agosti 17 katika viwanja vya Mlimani City.

Picha katika matukio ya jana

Huu ni msimu wa tatu wa michuano hiyo, ambapo katika usajili na ufunguzi, timu mbalimbali zimejitokeza kujisajili na kutakuwa na hatua za mtoano kisha robo fainali, nusu fainali na fainali.

Akifungua rasmi michuano, mwakilishi kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Malinde Lutiho Mahona amesema kuwa Serikali inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na East Africa Tv, East Africa Radio na kampuni ya Coca-Cola kupitia kinywaji chake cha Sprite kwa moyo wao wa kujitolea kukuza mpira wa kikapu nchini.

"Serikali ipo pamoja na nyinyi, inatambua faida kubwa iliyopo kwenye michezo ndio maana inapoona watu wenye moyo kama Coca-Cola, East Africa Radio & East Africa Tv . Tunatoa pongezi sana", amesema Mahona.

"Pia tunawaomba wadau wengine wawekeze katika viwanda vya michezo ili tupate vijana ambao Taifa zima linawaangalia, kwahiyo kwa sasa vijana onesheni vipaji vyenu katika mashindano haya", ameongeza.

Naye kwa upande wake, Mkurugenzi wa Umma na Mawasiliano wa Coca-Cola ambayo inazalisha kinywaji cha Sprite, Haji Mzee Ally amesema, "ahadi yetu kama Coca-Cola ni kuendelea kuwa mstari wa mbele hasa linapokuja suala la kuwasaidia vijana, katika kuendeleza vipaji vyao ambavyo vitaleta mabadiliko katika maisha yao".

Akaongeza, "tumelidhihirisha zaidi kupitia majukwaa mengine ya kuibua vipaji kama vile Coke Studio Afrika, East Africa Got Talent na mashindano ya COPA Coca-Cola."

Mpaka zoezi la usajili linakamilika katika viwanja vya Mlimani City, jumla ya timu 39 zimeshajisajili kwa ajili ya michuano hiyo inayotarajia kutimua vumbi hivi karibuni. Zoezi la usajili litaendelea tena Jumatatu ya Agosti 19.

Aidha wimbo maalum wa michuano ya Sprite Bball Kings 2019 umezinduliwa katika siku ya uzinduzi hii leo ambapo wasanii waliofanya wimbo huo, G Nako 'Warawara', Frida Amani na Chemical, walipata nafasi ya kuuzindua rasmi mbele ya wageni waalikwa na watu waliojitokeza.