Jumamosi , 25th Jun , 2016

Simba SC ina misimu minne mfululizo haijaonja raha ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara, hali ambayo imewafanya mashabiki wa msimbazi kuwa wanyonge mbele ya watani zao Yanga na sasa wanasubiri pengine furaha yao itarejeshwa na kikosi kinachosajiliwa sasa.

Laudit Mavugo wa Vital’O ya Burundi.

Kuna kila dalili katika hali isiyotarajiwa uongozi wa Simba kupitia kamati yake ya usajili wakati wowote kuanzia sasa ikamshusha nchini straika fundi wa mabao Laudit Mavugo baada ya kumaliza mkataba wake wakuitumikia timu ya Vital’O ya Burundi baada ya awali dili hilo kushindikana.

Tangu mwaka jana, Simba ilikuwa ikimuwania na kutangazwa imemalizana na Mavugo raia wa Burundi kila kipindi cha usajili kinapofika lakini mambo huaribika nahivyo sasa ikabidi isubiri hadi straika huyo alipomaliza mkataba wake msimu huu.

Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Simba ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema Mavugo atatua wakati wowote kuanzia sasa na tayari alisaini mkataba wa miaka miwili tangu msimu uliopita japo alishindwa kujiunga na wenzake kutokana na mambo fulani fulani ya baadhi ya watu ambao sasa hawana nafasi tena.

Mtoaji nyeti hiyo amesema mkataba huo uliigharimu Simba kiasi cha pesa taslimu za Kitanzania Shilingi milioni 36, lakini awali walibanwa na mambo ya mkataba wa straika huyo na timu yake hivyo kungoja hadi amalize mkataba huo kwanza.

Nukuu “Mavugo atawasili nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa kuwa ni mchezaji wetu na alisaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia Simba na fedha zilizotumika kwenye usajili wake ni shilingi milioni 36".

“Kwa sasa mkataba wake umekwisha kule katika timu yake aliyokuwa akiichezea, hivyo yupo huru na ni uhakika safari hii atakuja kuichezea Simba msimu ujao,” alisema bosi huyo.

Mavugo ana uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu na Simba inaamini atakuwa mkombozi wao msimu ujao na kuzima ngebe za wapinzani wao Yanga ambao wamekuwa wakitamba na kina Donald Ngoma na Amis Tambwe na sasa Mzambia Chirwa aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea katika klabu ya FC Platnum ya Zimbabwe.